Thursday, January 10, 2013

TUME YA KATIBA YATOA TAMKO KALI KWA WAANDISHI WA HABARI

Tume ya Mabadiliko ya Katiba imetamka rasmi kuwazuia waandishi wa habari kuhudhuria mikutano yake na makundi maalum, vikiwamo vyama vya siasa, inayoendelea kwa lengo la kukusanya maoni ya Katiba Mpya.

Kwa kauli hiyo ya Tume hiyo, sasa itategemea huruma na hisani ya makundi, ambayo yatakuwa tayari ‘kuwatafunia’ na ‘kuwalisha’ wanahabari mambo yaliyojiri, badala ya wao wenyewe kuyapata moja kwa moja na kwa uhalisia wake kutoka ndani ya mikutano hiyo.

Kauli ya kuwazuia waandishi wa habari kuhudhuria mikutano hiyo, ilitolewa na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Joseph Warioba, jijini Dar es Salaam jana, kabla ya kuanza mkutano kati ya tume yake na Chama cha Union for Multiparty Democracy (UMD).

Jaji Warioba alitoa kauli hiyo alipoulizwa na NIPASHE kama waandishi wa habari wangeruhusiwa kuingia ukumbini kusikiliza maoni ya UMD.

Alijibu kwa kifupi kwamba waandishi wa habari hawaruhusiwi kuhudhuria siyo tu katika mkutano huo juzi, bali katika mikutano yote kati ya Tume na makundi yote.

“Hamuwezi kuingia ukumbini (kwenye mkutano) kusikiliza maoni yanayotolewa. Siyo tu tuliwazuia jana (juzi), bali hata leo (jana). Pia na siku nyingine hamtaruhusiwa kushiriki,” alisema Jaji Warioba.

Mikutano kati ya Tume na makundi hayo ilianza juzi katika ofisi za Tume hiyo na katika kumbi tofauti za jengo la Karimjee, jijini Dar es Salaam.

Katika ofisi za Tume, mikutano hiyo inaongozwa na Jaji Warioba pamoja na mjumbe wa Tume hiyo, Profesa Mwesiga Baregu.

Katika kumbi za jengo la Karimjee, baadhi ya mikutano inaongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Tume, Jaji Augustino Ramadhan na maofisa wengine wa Tume hiyo.

Katika mikutano yote hiyo, baadhi ya maofisa wa Tume, wamekuwa wakiwazuia waandishi wa habari kuhudhuria.

No comments:

Post a Comment