Thursday, January 10, 2013

Askari polisi wauwawa huko Ngara

 Askari wawili wa Jeshi la Polisi wa Wilaya ya Ngara mkoani Kagera, wameuawa kwa kupigwa na wananchi wenye hasira na  gari lao kuchomwa moto, wakidhaniwa kuwa ni majambazi.

Tukio hilo lilitokea katika Kijiji cha Kasheshemisha, Kata ya Rugu Wilaya hiyo juzi saa 2:30 usiku.

Akitoa maelezo mbele ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Karagwe chini ya Mkuu wa Wilaya  hiyo,  Darry Ibrahim Rwegasira na ya Mkoa iliyoongozwa na Kamanda wa Polisi Mkoa huo,  Phillipo Kalangi na viongozi wengine wa serikali wilayani humo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kasheshemisha, Sadick Mohammed, alisema walipata taarifa kutoka Kijiji cha Rugu kuwa kuna majambazi  walifika majira ya saa 12:00 jioni na wakati wakijaribu kuondoka, wanakijiji waliweka kizuizi barabarani na kuwaamuru wasimame.

Mihamed alisema watu hao hawakutii amri na kupita kwa nguvu katika eneo hilo ndipo walipoamua kupiga simu kwa mwenyekiti huyo ambaye naye alitoa taarifa  kwa wananchi wake na kuziba barabara kwa mawe.

Alisema  gari lao lilipofika Kijiji cha Kasheshemisha, lilikuta mawe barabarani na kushindwa kupita ndipo wananchi waliwaamuru  wajisalimishe, lakini walikaidi na kuanza kufyatua risari hewani huku wakitafuta njia ya kuwawezesha kutoroka.

Alisema walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa wawili na kutokana na hasira ya kurushiwa risasi, waliwapiga hadi kuwaua kisha walipopekua ndani ya gari walikuta meno saba ya tembo.

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, hasira za wananchi zilipanda zaidi walipogundua mwenzao amejeruhiwa na risasi na kuamua kuyatoa meno hayo ya tembo saba na kulitekeleza gari  hilo lenye namba za usajili T.654 BNB.

Mohamed alisema mwanakijiji huyo, Jovinary Joseph aliyejeruhiwa na risasi kwenye kiganja, alikimbizwa Hospitali Teule ya Wilaya ya Karagwe ya Nyakahanga kwa matibabu.

No comments:

Post a Comment