Monday, January 21, 2013

Ajali yaua mmoja MBEYA.




Mtu mmoja amekufa papohapo na wengine 48 kujeruhiwa vibaya baada ya basi walilokuwa wakisafiria kutoka Jijini Mbeya kwenda Dar es Salaam kupinduka kwenye mteremko mkali wa Mlima Inyara nje kidogo ya Jiji la Mbeya.

Ajali hiyo mbaya ilitokea jana majira ya saa 1:30 asubuhi ikihusisha basi la kampuni ya Nganga Express lenye namba za usajili T 413 AVU lililoondoka Mbeya majira ya saa 1:00 kuelekea Dar es Salaam.

Akisimulia jinsi ajali hiyo ilivyotokea, dereva wa basi hilo, Alex Bunyinyiga alisema alipofika kwenye mteremko wa mlima Inyara, mahali ambapo pia kuna kona kali, aliona lori kubwa lililokuwa limeegeshwa upande wa kulia wa barabara.

Alisema alipolikaribia lori hilo, ghafla lilitokea gari lingine aina ya Fuso ambalo lilipita lori lililoegeshwa na kumfuata upande wake, hali ambayo ilisababisha watake kugongana uso kwa uso.

“Baada ya kuona tunaenda kugongana uso kwa uso, niliamua kukwepesha gari langu upande wa lori lililokuwa limeeegeshwa upande wa kulia kwangu na nikafanikiwa kulipita lori hilo kwa upande wake wa kulia, lakini nilipojaribu kurudisha gari langu likae barabarani liligoma na ndipo likapinduka,” alisema Bunyinyiga.

Shuhuda mwingine wa ajali hiyo, Noa Elias alisema chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa lori aina ya fuso ambaye aliamua kulipita lori lililoharibika barabarani bila tahadhari na kutaka kugongana uso kwa uso na basi la Nganga.

Muuguzi wa Zamu katika Hospitali ya Rufaa Mbeya, Bilhuda Feruz amethibitisha kupokea majeruhi 48 na wanane kati yao wamelazwa na hali zao zinaendelea vizuri.

Hata hivyo, takwimu hizo zimetofautiana na zile zilizotolewa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Diwani Athuman ambaye alidai kuwa majeruhi walikuwa ni 53 nwa kwamba 45 kati yao walitibiwa katika Hospitali ya Rufaa na kuruhusiwa huku majeruhi wanane wakilazwa hospitalini hapo kwa matibabu zaidi.

Kamanda Diwani alimtaja mtu aliyepoteza maisha katika ajali hiyo kuwa ni Enock Lwila mkazi wa Mama John Jijini Mbeya.

Alisema marehemu huyo alikuwa na Sh. milioni 13 mfukoni ambazo ziliokolewa na askari waliowahi kwenye eneo la tukio.

Kamanda Diwani alisema kuwa kwa sasa fedha hizo ziko salama mikononi mwa Polisi na kuwa baada ya kupatikana kwa ndugu halali wa marehemu atakabidhiwa.

 
CHANZO: NIPASHE     

No comments:

Post a Comment