Thursday, January 10, 2013

Nyoso Wa SIMBA atemwa safari ya OMAN



 

  Mabingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Simba ya jijini Dar es Salaam, wamemtosa beki Juma Nyosso katika safari yao ya Oman iliyoanza kwa mafungu jana kutokana na kosa la kutotii masharti aliyopewa na uongozi wa klabu hiyo.

Simba iliondoka jijini Dar es Salaam jana na kikosi cha wachezaji 14 kuelekea Oman kwa ajili ya kuweka kambi ya wiki moja ya kujiandaa na Ligi ya Kuu ya Tanzania Bara na Ligi ya Klabu Bingwa Afrika.

Wachezaji wengine waliobaki kuiwakilisha Simba katika Kombe la Mapinduzi Zanzibar na walio katika kambi ya timu ya taifa (Taifa Stars) wataungana na wenzao Oman baada ya kumaliza majukumu yao.
Waliopo katika kikosi cha Stars kilichosafiri jana kwenda Ethiopia kucheza mechi ya kimataifa ya kirafiki kesho dhidi ya wenyeji ni kipa Juma Kaseja, Amir Maftaha, Mrisho Ngassa, Mwinyi Kazimoto, Shomari Kapombe na Amri Kiemba.

Waliobaki na timu yao kusubiri kumalizika kwa michuano ya Kombe la Mapinduzi inayoendelea visiwani Zanzibar ni Haruni Athuman, Abdalah Seseme, Miraji Adam, Julius Mkude na Hassan Singano.

Nyosso alirudishwa kucheza katika kikosi cha vijana wa U-20 wa klabu hiyo kutokana na utovu wa nidhamu na kushuka kwa kiwango chake, jambo ambalo beki huyo wa kati hajalitimiza.

Akizungumza na NIPASHE jana, Katibu wa Simba, Evodius Mtawala alisema Nyosso ameachwa na hatarudishwa kikosini hadi pale atakapotekeleza masharti.

"Kuna baadhi ya vitu tumesimamisha kwenye mkataba wake ikiwamo mshahara," alisema Mtawala.
Alisema atakapoanza kuvitekeleza atarejea kupata mahitaji yote kama ilivyo kwa wachezaji wenzake.

Mtawala alisema msimamo wa Simba uko pale pale kwamba beki huyo, ambaye ameripotiwa kutumia muda wake nje ya kikosi kucheza mechi za mchangani, ni lazima aende akaripoti kwenye timu ya vijana na akaonya kwamba kama ataendelea kukaidi agizo ataangukia pabaya.

Alimtaka mlinzi huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Tanzania Bara aache kusikiliza ushauri mbaya na badala yake atimize masharti ya ajira yake kwa manufaa yake mwenyewe.

No comments:

Post a Comment