Na;Dovakmwene John Mscheshi
Kifo ni kitu kinachoweza kumtokea mtu yoyote na wakati wowote kwani tunaamini ni mipango ya Mungu. Kifo hutokea katika mazingira tofauti ikiwa ni pamoja na maradhi, ajali mbalimbali, vita/mapigano, ugomvi na kadhalika.
Vifo vipo vya ghafla pasipo kutarajia,
vingine vikitokana na kuugua muda mfupi au mrefu. Mtu anapofariki
shughuli za mazishi huandaliwa ambapo waombolezaji hukusanyika nyumbani
kwa marehemu au sehemu iliyopangwa na wanafamilia kwa msiba.
Pale kwenye maombolezo huwa na
pilikapilika nyingi huku ratiba ya maandalizi ikitangazwa kila
inapobidi. Waombolezaji huonekana katika makundi wakiteta huku wengine
wakiwa wamejawa na simanzi.
Pamoja na ukweli huo, tabia hizi
hazipendezi. Kwa mfano, lipo jambo moja au niseme tabia ambayo
imezoeleka kwa waombolezaji wengi kuonekana wakijadili zaidi chanzo cha
kifo cha marehemu badala ya kutafakari hatma yao waliobaki duniani na
kumuombea aliyetangulia mbele za haki.
Kwa maneno mengine, wapo watu wanaogeuza
msiba kama vijiwe vya kumjadili marehemu. Na watu hawa, hata wakati wa
uhai wake hawakuwa kusema juu yake hadharani penye kadamnasi ya watu,
lakini leo kafariki wanazusha hata yale yaliyofichika. Hebu tujiulize,
hivi yanahusu? Na kwanini wanadamu tuko hivi? Hii ni kasoro kubwa sana
yafaa tubadilike.
Utasikia fulani wakati wa uhai wake
alikuwa anaringa sana. Ebo! Ulitaka afanyeje. Hivi hujui maringo ni afya
na kinyume chake ni kasoro? Kuringa ni kujisikia furaha kwa uhai wako.
Ndio, usibishe.
Mara utasikia fulani alikuwa kiruka njia,
alipenda sana wanaume au wanawake, alipenda sana wake au waume za
watu…Oh, ameacha watoto wa baba tofauti, amekufa na gonjwa baya, eti
angezingatia ushauri wa daktari yasingemsibu hayo, ili mradi ni maneno
ya hovyo, kisa anayezungumzwa ameshajifumzikia.
Wengine utasikia eti laana ya baba au mama
yake ndio imemuua. Ili mradi mtu atoe neno kinywani mwake kufurahisha
jopo pale kwenye maombolezo. Hili siyo jambo zuri hata kidogo, hasa
ikizingatiwa kuwa kila mtu anayo mapungufu yake na hakuna atakayeishi
milele nikiamini kile alichowahi kuniambia bibi yangu kuwa “Uyana nyi
maseiyano” yaani “Dunia ni mapishano”.
Tabia nyingine inayokera wakati wa msiba
ambayo wengi bado wanaiendekeza ni kule baadhi ya ndugu kugombea mali za
marehemu zikiwemo nguo zake. Eti kufa kufaana na kwamba aliyekufa kafa
hivyo mali zake ni halali kwa wengine. Lo! Makubwa kwani madogo yana
unafuu.
Nimewahi kushuhudia ndugu wakichukua nguo
za marehemu kwa kuzificha na kuondoka nazo, tena mwili wa marehemu ukiwa
bado chumba cha maiti hospitalini. Yaani mwili haujazikwa, tayari watu
wanajigawia mali zake. Ni tabia mbaya sana hii. Wenye tabia hii
wasidhani ni kirahisi hivyo, yapo madhara yake. Kwanini mtu asisubiri
kupewa mali chini ya taratibu za kifamilia?
Lingine ambalo halina sura nzuri
walifanyalo wanadamu ni kule kukimbilia kuuona mwili wa marehemu wakati
hapa alipokuwa mgonjwa hakuwahi kwenda kumjulia hali achilia mbali
kumsaidia fedha za matibabu. Hukimbilia kuona kafa na afya yake au
kakonda? Acheni jamani, mzaha huu, ni dhambi.
Mpenzi msomaji, hebu niulize; lipi ni jema
katika haya mawili:- kumtembelea mgonjwa na ikibidi kumsaidia fedha za
matibabu au kule kwenda mchanga rambirambi baada ya kufa?
Wapo wale ambao hawakujua fulani alikuwa
mgonjwa, lakini wakasikia amefariki. Lakini wengine, pengine mahasimu
waliowahi kukwaruzana, wakisia fulani kafa huachia; “acha afe”. Yaani
hawaoni kwamba hiyo ni njia yao pia. Huu siyo ubinadamu. Maisha ya mtu
yanapotoweka lazima usikitike kwani hutamuona tena katika maisha haya ya
kidunia. Na utambue nawe kifo kinakusubiri.
Nakumbuka bibi mzaa mamangu wakati wa uhai
wake kila nilipomtembelea alikuwa anafurahi sana pale ninapompelekea
zawadi ambapo husema; “Afadhali uniletee watati ningali hai, kwani
nikishafumba macho(kufa) utakachoniletea ni bure”. Yalikuwa ni maneno
yaliyobeba ujumbe mzito sana.
Ndio maana ni muhimu sana hata pale
mwenzako anapokuwa mgonjwa yafaa tumhudumie kwa nguvu zote, tumsaidie
chakula, dawa badala ya kusubiri azimike ndipo tupige mikono mifukoni
kutoa rambirambi.
Sisemi watu wasitoe rambirambi, la hasha.
Ninachosema hapa ni kwamba tutizame mazingira yenyewe, kama ni kifo cha
ghafla ni sawa. Lakini kama ni kifo kinachotokana na maradhi tusaidiane
wakati wa uhai badala ya kubezana. Pengine msaada wako unaweza
kumsogezea mgonjwa maisha akakamilisha mipango yake duniani au hata
akapona kabisa. Maisha Ndivyo Yalivyo.
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment